Thursday, October 19, 2023

ATCL YATAKIWA KUPATA FAI



 

Serikali imelitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuhakikisha linapanga mikakati madhubuti itakayoliwezewesha kukua na kujiendesha kwa tija  baada ya uwekezaji mkubwa unaofanywa kupitia ununuzi wa ndege za masafa mafupi, ya kati na marefu.

 

Akizungumza wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Pili la Wafanyakazi mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema ununuzi wa ndege hizo unaofanywa pamoja na maboresho katika viwanja unatarajiwa kuongeza tija katika usafiri wa anga nchini.




 

“Kama Serikali tunategemea ndege hizi 14 zilizonunuliwa ziwe na matokeo chanya ambayo yataonekana na niwahakikishie kuwa ndege zilizobaki Serikali itahakikisha zinakuja ili Shirika liendelee kupiga hatua”, amesema Kambelenje.

 

Mkurugenzi Kambelenje ameipongeza ATCL kwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwawezesha wataalam wa kampuni hiyo kufanya matengenezo ya ndege wenyewe kwa  matengenezo makubwa (C Check) hapa nchini hali inayookoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingelipwa kwa makampuni ya nje ya nchi.

 

Aidha, Kambelenje ameitaka ATCL kuhakikisha inaboresha huduma kwa wateja ili kuvutia wateja wengi zaidi kutumia Shirika hilo kwa safari za ndani na nje ya nchi.

 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imeweza kutengeneza mifumo mbalimbali ya tehama inayotumika kwenye mauzo ya tiketi pamoja kuingia makubaliano na mashirika mengine ya kimataifa ili kupata wateja kwenye maeneo ambayo ATCL haitoi huduma.

  

Mkurugenzi Matindi amebainisha kwamba, ATCL imefanikiwa kuongeza vituo vya safari kutoka vine (4) hadi kufikia vituo 15 vya ndani na 11 vya nje ya nchi.

 



Baraza la Wafanyakazi wa ATCL linakutana kwa siku mbili mkoani Morogoro ambapo pamoja na kufanya tathimini ya utendaji Shirika hili pia litajadili Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano (Corporate Strategic Plan 2022/23 – 2026/27) wa Kampuni hiyo.

 

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Uchukuzi)

CNG IPEWE KIPAUMBELE KUENDESHA MITAMBO NA MAGARI NCHINI- KAMATI YA BUNGE

CNG IPEWE KIPAUMBELE KUENDESHA MITAMBO NA  MAGARI NCHINI- KAMATI YA BUNGE


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuweka kipaumbele katika kusambaza Vituo vya Nishati ya Gesi Iliyoshindiliwa (CNG) inayotumika katika kuendesha mitambo na magari nchini ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mafuta pale zinapotokea.

Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 18, 2023  jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mathayo David wakati Kamati hiyo ilipopokea taarifa ya Wizara ya Nishati, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kuanzisha vituo hivyo. 





“Tunashauri Serikali iweke kipaumbele katika matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na matumizi mengine ili Watanzania waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi,” amesema Mwenyekiti wa Kamati,  Mathayo David.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mathayo ameipongeza Serikali kwa mikakati mizuri ya uanzishwaji wa karakana za kubadili mifumo ya matumizi kutoka kwenye mafuta na kwenda kwenye gesi asilia kwenye magari hali  inayochochea matumizi ya gesi asilia nchini kwa wingi. 

"Uwepo wa karakana hizi kwa wingi utarahisisha utoaji wa huduma za ubadilishaji mifumo na ukarabati wa hitilafu kwa muda mfupi na karakana hizi zitumie teknolojia ya kisasa wakati wa kubadili magari na mitambo,” ameeleza Mhe. Mathayo.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imepokea ushauri wote uliotolewa na kamati ili kuweza kuboresha Sekta ya Nishati nchini.  

Amesema, Wizara imedhamiria kuchochea matumizi ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa kwa maeneo pia  yaliyo mbali na mtandao wa mabomba pamoja na matumizi ya gesi hiyo kwenye magari kwa kuwa na vituo vingi vya kujazia gesi kwenye magari. 


Viongozi mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga na Watendaji kutoka Wizara na Taasisi.